Available in print form, Tunguu Reference Library
Utafiti huu unahusu Ugumu wa kufundisha Stadi ya Kusikiliza kwa Wanafunzi Wageni Wanaojifunza Kiswahili: Mfano Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA). Utafiti ulikuwa na lengo la kuangalia mambo makuu matatu. Kwanza, kubaini mbinu wanazotumia walimu wakati wa kufundisha stadi ya kusikiliza. Pili, kupambanua ugumu unaowakabili walimu wa Idara ya Kiswahili kwa Wageni katika kufundisha stadi ya kusikiliza. Tatu kupendekeza mikakati itakayoweza kusaidia kuimarisha stadi ya kusikiliza. Utafiti ulifanyika Idara ya Kiswahili kwa Wageni (SUZA). Utafiti uliongozwa na “Modeli ya Ufundishaji Lugha Kimaakazi” kama ilivyoasisiwa na Echevarria, Vogt na Short, 2000; 2013).Utafiti ulitumia mbinu ya ushuhudiaji, mahojiano na uchambuzi wa nyaraka katika kupata data. Sampuli ya watoa taarifa walikuwa ni walimu wanaofundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni katika kiwango cha kati. Matokeo yanaonesha kuwa walimu hutumia mbinu zifuatazo: Kusikiliza redio na kisha kujibu maswali, kusikiliza nyimbo na baadaye kujibu maswali, kufanya imla, kutumia simu kusikiliza habari na kisha kujibu maswali, kualika mgeni, ziara za kimasomo, kumsikiliza mwalimu kusoma matini na baadaye kufanya mazoezi ya oral (kutamka) kufundisha stadi ya kusikiliza. Kadhalika, matokeo ya utafiti huu yanaonesha kwamba upo ugumu unaowakabili walimu katika kufundisha stadi ya kusikiliza. Ugumu huo ni pamoja na kuchukua muda katika matayarisho, ukosefu wa maabara ya lugha na vifaa vingine vya ufundishaji, mtaala kutoelekeza ufundishaji wa stadi ya kusikiliza, kukosekana kwa mafunzo ya jinsi ya kufundisha stadi ya kusikiliza kwa walimu, mazingira ya darasa, utayari wa wanafunzi na tofauti ya kiwango cha uelewa wa wanafunzi. Aidha, ili kuimarisha ufundishaji wa stadi ya kusikiliza imependekezwa mikakati ifuatayo: Mabadiliko ya mtaala na vitabu vya kufundishia, mafunzo kwa walimu yatolewe mara kwa mara, utumiaji wa teknolojia na vifaa vya kisasa, kupewa hadhi sawa stadi zote za lugha na kufanya tathmini katika stadi ya kusikiliza. Mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na utumiaji wa ufarafuzi wa vifaa, kufanya utafiti katika stadi nyingine za lugha kama vile kusoma, kuzungumza na kuandika, kuangalia ugumu wa stadi ya kusikiliza katika viwango vingine. Mapendekezo hayo yatachangia kwa kiasi kikubwa ufundishaji wa Kiswahili ikiwa lugha ya kigeni utafundishwa vizuri kwa kuzingatia stadi zote za lugha bila ya kuibagua hata moja hususan stadi ya kusikiliza.