Available in print form, Tunguu Reference Library
Utafiti huu unahusu “Muundo wa Lugha katika Mashairi ya Watungaji Wateule wa Zanzibar”. Diwani nne za watungaji wawili wa Zanzibar zilichambuliwa. Diwani hizo ni Kina cha Maisha ya Mohamed (1984) na Jicho la Ndani ya Mohamed (2002). Diwani nyengine ni Andamo iliyoandikwa na Ghassani (2016a) na Siwachi Kusema pia ya Ghassani (2016b). Utafiti huu ulifanywa katika Wilaya ya Magharibi A, Magharibi B na Wilaya ya Kusini, Unguja, Zanzibar. Data za msingi zilipatikana kwa njia ya maktaba, usaili kwa wahakiki wa fasihi na hojaji kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Zanzibar. Njia ya maktaba iliwezesha kupata data nyingi za msingi zilizotimiza malengo ya utafiti. Malengo hayo ni kuchunguza vijenzi vya lugha katika ngazi ya fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki, vilivyoyajenga mashairi ya watungaji wateule wa Zanzibar kimaana na kiujumi. Aidha, utafiti ulichunguza ukiushi wa kanuni za kisarufi katika mashairi hayo na jinsi vijenzi vya lugha vilivyopambanua mtindo. Nadharia ya Umuundo na Umuundoleo zilitumika katika uchambuzi wa data. Utafiti umeonesha kuwa watunzi wote wamevitumia vijenzi vya lugha katika ngazi ya fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki kuyajenga mashairi yao. Watunzi wote wamevitumia vijenzi vya lugha kwa kuzingatia kanuni za lugha kwa usahihi kulingana na muktadha, mazingira na wakati. Aidha, wamevisarifu vijengo vya lugha kuimarisha sanaa zao kiujumi na kimaana kwa kuzingatia sifa za lugha ya kishairi inayoendana na mkwepo wa sarufi. Hali hiyo imedhihirisha kuwa upo ufungamanifu kati ya vijenzi vya kimuundo na ushairi, kwa kuwa vijenzi hivyo ndivyo vilivyotumika kuyajenga mashairi ya watungaji wateule wa Zanzibar.