Available in print form, Tunguu Reference Library
Utafiti huu ulifanyika kisiwani Unguja, katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, taasisi mbili zilichanguliwa kushiriki katika utafiti huu. Moja ya taasisi hiyo ni ya kiserikali na nyengine ni taasisi binafsi. Lengo kuu la utafiti huu ni kutathmini mbinu wanazozitumia walimu katika kufundisha stadi ya kuandika Kiswahili kama lugha ya kigeni kwa kuzingatia kipengele cha utungaji. Watafitiwa katika utafiti huu walikuwa ni walimu wanaofundisha Kiswahili kama lugha ya kigeni katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Taasisi ya Kiswahili na Kiswahili na Utamaduni (KIU) ambazo kieneo zote zinapatikana Zanzibar. Mbinu mbalimbali za kukusanyia data ambazo ni usaili, dodoso na ushuhudiaji zilitumika katika kupata data zenye uhakika na zenye kuaminika. Matokeo ya utafiti yamebainisha kuwa, ni kweli kuna mbinu ambazo walimu wanazitumia katika kufundishia stadi ya kuandika. Walimu wanatumia mbinu kama vile mbinu ya picha, hadithi, ziara za kimasomo, barua na mbinu jumuishi/mseto katika kufundisha stadi ya kuandika Kiswahili kama lugha ya kigeni hasa katika kipengele cha utungaji. Kutokana na matokeo na mapendekezo ya utafiti pamoja na watafitiwa imegundulika kwamba walimu hawana mafunzo ya kutosha juu ya stadi za lugha, pia muamko katika ufundishaji wa stadi ya kuandika ni mdogo sana ingawa mbinu za kufundishia zipo wazi bado kunahitajika ushajihishaji wa hali ya juu kwa wanafunzi. Katika utafiti huu, mtafiti alipendekeza taasisi zenye dhima ya kufundisha Kiswahilikama lugha ya kigeni Zanzibar, zijaribu kuandaa warsha za mafunzo ya mbinu za kufundishia stadi za lugha hasa stadi ya kuandika.Hali hii itasaidia walimu katika kuboresha ufundishaji wao wa stadi hii na stadi nyengine za lugha. Mwisho kabisa, mtafiti alishauri tafiti nyengine zifanyike ili kuziba pengo lililoachwa na watafiti wengine, na watafiti wajikite zaidi katika stadi za lugha hasa Kiswahili kama lugha ya kigeni.