Full text can be accessed at
http://www.ajol.info/index.php/ksh/article/view/64856
UKIMWI umeendelea kuleta changamoto katika maisha ya binadamu. Ni janga ambalo linagusa maisha ya kila siku ya binadamu katika nchi nyingi na hasa zilizo fukara. Kutokana na kugusa sehemu mbalimbali za maisha, janga hili limejadiliwa katika nyanja mbalimbali za kitaaluma ikiwa ni pamoja na tabia na mahusiano ya watu (Nelkin na wenzie 1991). Katika Tanzania, UKIMWI umejadiliwa kihistoria (Kaijage, 1993) na hata katika sanaa mbalimbali ikiwamo lugha na fasihi (Mutembei 2001; Mutembei na wenzie, 2002) Kuhusu lugha na fasihi kwa ujumla, UKIMWI ndio ugonjwa ambao kwa muda mfupi umejitokeza katika maandishi zaidi kuliko magonjwa mengine yoyote yale. Hata katika nchi za ki-Magharibi kwa mfano, kifasihi UKIMWI umejitokeza katika maandishi zaidi kuliko saratani. Nchini Marekani, UKIMWI umejadiliwa zaidi katika maandishi kuliko kifua kikuu katika miaka ya 1990 kama Goldstein (na wenzie) wanavyosema katika nukuu hii:
Wala sio kifua kikuu, lile gonjwa, kigaga cha magonjwa ya mlipuko, ambalo kwa kulinganisha na magonjwa mengine lenyewe linaweza kutoa maandishi mengi ya kifasihi kwa muda mfupi.
[Not even tuberculosis, that most “aesthetic” of epidemics, produces a comparable outpouring in so short a time].
(Goldstein katika Nelkin na wenzie 1991: 17)
(Tafsiri ya mwandishi).
Mbali na kulinganishwa na kifua kikuu, UKIMWI nchini Marekani, unajitokeza zaidi katika maandishi kuliko homa ya manjano, kipindupindu na magonjwa mengine mengi. Kwa muda mfupi tu, UKIMWI umejitokeza katika maandishi ya kifasihi sawa na gonjwa la tauni lilivyojitokeza katika maandishi ya namna hiyo huko Ulaya. Kwa sababu ya hali hii, janga hili linavuta hamu ya kitaaluma ya kutaka kutafiti ni kwa vipi na kwa kiasi gani limejipenyeza katika sanaa za jamii, na hususani limejipenyeza katika tanzu zipi za fasihi ya jamii. Kwa mfano, ni kwa kiasi gani UKIMWI umejipenyeza katika fasihi ya Kiswahili? Ni kwa namna gani athari za UKIMWI zinaweza kuonekana kama kipengele cha ujumi katika maisha ya Watanzania? Katika fasihi, ni tanzu zipi zimeitikia mguso wa janga hili na kulielezea kisanii? Na maelezo hayo yanamaanisha nini katika maendeleo ya utanzu husika na kwa fasihi kwa ujumla? Katika mantiki hii, makala haya yanajadili jinsi utanzu wa methali unavyoguswa na janga hili.