Tamthiliya hii ya Nelson Mandela inatupatia fursa nyingine ya kujifunza kuhusu historia ya ukombozi wa nchi ya Afrika Kusini, pamoja na nafasi ya nchi wahirika kama vile Tanzania, walivyosaidiana bega kwa bega hadi Afrika ya Kusini ikawa huru kupitia kiongozi mzalendo na Baba wa Taifa, Nelson Mandela. Kupitia tamthiliya hii, msomaji atajifunza mambo mengi ikiwemo uzalendo, kujitoa muhanga, umajumui wa Kiafrika kwa kutaja kwa uchache. Tamthiliya hii imechanganya mbinu mbalimbali za kiutunzi ikiwemo "tamthiliya ya Kiafrika" (inayotumia Sanaa za maonesho za Kiafrika kama vile ngoma); "tamthiliya ya Kiaristotle" (kwa maana inatumia mbinu za utunzi wa tamthiliya ya kale ya Kigiriki ikiwamo matumizi ya korasi); na "tamthiliya ya Kibrecht" (kwa maana inatumia mbinu za filamu, bakigraundi, mabango nk). Tamthiliya hii imechotarisha mikabala hiyo mitatu ya kiutunzi ambayo inatawala katika utunzi na ubunifu wa tamtiliya (plays).
Nelson Mandela ni drama/tamthiliya/mchezo wa kuigiza unaomsawiri Rais wa kwanza mzalendo wa Taifa la Afrika Kusini, ambaye ni Baba wa Taifa kwa Waafrika Kusini. Nelson Mandela alizaliwa mwaka 1918 na alifariki mwaka 2013 na kuzikwa kijijini kwake Qunu huku watu mbalimbali duniani wakihudhuria maziko yake. Maadui na mahasimu walipatana wakati huu kwa kuwa Nelson Mandela aliweza kuwakutanisha ana kwa ana. Mandela ni mfano mzuri wa kuigwa kwani alitimiza amri ya Mwenyezi Mungu ya ‘KUWASAMEHE’ wote wanaokuudhi. Nelson Mandela ni mwanadamu wa pekee ambaye aliweza kulitimiza jambo hilo. Aliwasamehe wale wote waliomkosea kwa kumfunga kwa kumwonea na pia kuwatedea unyama watu weusi huko Afrika ya Kusini. Mungu ailaze roho ya Nelson Mandela mahali pema peponi – amina! Daima utakumbukwa na Watanzania, Waafrika Kusini na watu wote ulimwenguni.