dc.description |
Matumizi ya wingilugha yanazidi kuongezeka katika mandharilugha ya miji mbalimbali ulimwenguni. Kutokana na ongezeko hilo, ni hali ya kawaida kuona maandishi ya kijamiilughaulumbi katika eneo la mandharilugha. Katika nchi ya Tanzania kwa mfano, tafiti zinadhihirisha kuwapo kwa maandishi ya kijamiilughaulumbi kwenye miji kama vile Dar es Salaam, Arusha, Iringa, Kagera, Manyara na Mbeya. Aidha, maandishi ya kijamiilughaulumbi katika mandharilugha yanaweza kuwa katika aina tofautitofauti kutegemeana na jamiilugha husika. Kwa mujibu wa Reh (2004), maandishi hayo yanaweza kuainishwa katika makundi manne ambayo ni urudufishaji fumbato, urudufishaji usofumbato, urudufishaji achanishi, na ujalizaji. Lengo la makala hii ni kuchunguza aina za maandishi ya kijamiilughaulumbi katika mandharilugha ya jiji la Dar es Salaam kwa kutumia mkabala huo wa Reh (2004). Data zilizotumiwa katika utafiti huu ni maandishi yaliyokusanywa kwa njia ya upigaji picha katika maeneo ya Posta na Kariakoo jijini Dar es Salaam. Matokeo ya utafiti huu yanadhihirisha kuwapo kwa aina za ujalizaji pamoja na urudufishaji usofumbato huku aina za urudufishaji fumbato na achanishi zikiwa hazijadhihirika. |
|