Description:
Makala hii inajadili dhana ya utendaji wa fasihi simulizi mtandaoni. Kiini cha makala hii ni hoja kuwa uainishaji wa fasihi hivi sasa, yaani fasihi simulizi na fasihi andishi, umekitwa katika aina za uwasilishaji, ambazo ni uwasilishaji wa kimazungumzo na wa kimaandishi. Ugunduzi wa intaneti, na kuingia kwa teknolojia hiyo katika vifaabebe kama vile simu na sleti2 kwa kutumia programu mbalimbali za kuwasiliana, umewezesha mawasiliano ya kimaandishi ya papo kwa papo au yasiyo ya papo kwa papo. Mawasiliano hayo yamechangia kuibuka kwa lugha ya kipekee ambayo sifa zake hazifanani na sifa ya lugha ya kimazungumzo wala lugha ya kimaandishi. Licha ya kuwa na lugha ya kipekee, baadhi ya tanzu za fasihi simulizi, kwa namna ya kipekee, zimekuwa zikitendeka mtandaoni kwa kutumia lugha hiyohiyo. Utafiti huu umefanyika kwa kutumia Nadharia ya Utendaji bila kuathiri nafasi na umuhimu wa matini katika kazi za kifasihi.3 Data za utendaji wa vitendawili mitandaoni zilikusanywa, zilichambuliwa, na matokeo yake yanawasilishwa katika makala hii. Kwa kutumia utendaji wa vitendawili vya Kiswahili mtandaoni, ninapendekeza liundwe tawi jipya la fasihi ambalo litafumbata sifa za aina hiyo ya mawasiliano.