dc.description |
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa ni kubaini dhima ya tamathali za semi katika
nyimbo za siasa za Wagogo. Data zilikusanywa kutoka jamii ya kabila la Wagogo
wanaoishi mkoa wa Dodoma, wilaya ya Kongwa kata ya Mtanana. Nyimbo
mbalimbali za siasa zilikusanywa toka kwa wasanii mbalimbali wa kata ya Mtanana
na kwa baadhi ya wananchi wa kata hiyo walihojiwa. Vilevile, zoezi la ushuhudiaji
wa nyimbo za siasa ulifanywa na mtafiti. Aidha, mijadala mbalimbali ya vikundi
ilifanywa. Nyimbo zilizokusanywa zilichambuliwa ili kuona jinsi tamathali za semi
zinavyojitokeza, athari zake na dhima yake kwa jamii. Mbinu ya maelezo ilitumika
katika kufanya utafiti huu na data zilichambuliwa kwa kutumia nadharia ya uhalisia
wa kijamaa na nadharia ya U-Marx. Kadhalika, makala mbalimbali zilisomwa ili
kupata data zinazohusiana na utafiti huu.
Utafiti huu umebaini kuwa tamathali za semi zinazotumiwa na wasanii wa nyimbo
za siasa toka katika jamii ya Wagogo hazitumiwi bure, bali zina dhima mahususi.
Imebainika kuwa, tamathali za semi zinazojitokeza katika nyimbo za siasa za
Wagogo zimejitokeza kwa namna mbalimbali zikiwa na dhima ya kuburudisha,
kukosoa, kuokoa muda, kuhamasisha, kuweka msisitizo wa mambo, kuepusha
migogoro, kuendeleza utamaduni na kujenga taswira. Utafiti huu ulibaini kuwa,
wasanii wa nyimbo za siasa wamepevuka kisanaa kwani wanaweza kuweka vionjo
vya kifasihi hasa katika matumizi ya lugha kwa kuweka tamathali za semi katika
nyimbo zao kwa malengo maalum ambapo tamathali hizo za semi huleta athari
mbalimbali kwa jamii. |
|