dc.description |
Tasnifu hii inayoitwa ―Falsafa ya Riwaya za Shaaban Robert na Euphrase
Kezilahabi katika Muktadha wa Epistemolojia ya Kibantu‖ imechunguza namna
maarifa ya Wabantu yanavyojitokeza katika riwaya za Shaaban Robert na Euphrase
Kezilahabi. Uchunguzi huo umezingatia vipengele mbalimbali kama vile uchawi,
tambiko, imani au fikra zao kuhusu roho na kifo, moyo, Mungu, mwanya, uzazi,
utoaji majina, uganga na ardhi.
Taarifa zilikusanywa kwa njia ya mahojiano, majadiliano katika vikundi, mapitio ya
maandiko na ushuhudiaji. Taratibu za ukusanyaji wa data ziliongozwa na mkabala
wa kifinomenolojia, wakati uchanganuzi wa taarifa uliongozwa na mkabala wa
kiepistemolojia. Finomenolojia ni mkabala maarufu katika utafiti wa kitaamuli;
epistemolojia ni mkabala mpya katika uchambuzi wa kazi za fasihi. Matumizi ya
mkabala huu yamedhihirisha kuwa Wabantu wana namna yao ya kupata maarifa
ambayo ni kupitia kani-uhai toka kwa Mungu wao. Wazee walio hai ndiyo chanzo
cha maarifa hapa duniani kwa kuwa wana uwezo wa kuwasiliana na wahenga wao
kwa urahisi zaidi. Aidha, kujua kwao kumefungwa kwenye duara linalofanywa na
kani-uhai toka kwa Mungu, kuja kwa wahenga, kisha kwa watu walio hai na kurudi
tena kwa Mungu. Mungu ndiye chanzo kikuu cha kani-uhai. Aliye nje ya duara hili
linaloundwa na kani-uhai, hawezi kuwa na maarifa ya kaida za jamii yake. Kwa
Wabantu, maarifa ni kujua asili ya kani-uhai na athari zake. Jambo hili hutokana na
uzoefu wa muda mrefu wa kaida za jamii husika; pamoja na kudumisha mila na
desturi zinazoimarisha uhusiano uliopo ndani ya duara la maisha.
Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa; pamoja na kuyaweka mawazo ya Falsafa za
Ulaya na Asia katika maandishi yao, kwa kiasi kikubwa, kazi za Shaaban Robert na
Euphrase Kezilahabi zinawasilisha maarifa halisi ya Wabantu. Utafiti umebaini kuwa
maarifa ya Wabantu yanaegemea katika misingi ya kiontolojia. Hivyo basi, ontolojia
ndiyo kiini cha epistemolojia ya Kibantu. Katika kudhihirisha hili, vigezo
vinavyotumiwa na Wabantu katika kumbainisha mtu vimewekwa bayana.
Utafiti pia umebaini kuwa waandishi hawa wawili hawakumwacha mtu akiwa
hewani, bali baada ya kumbainisha kwa mujibu wa maarifa yao, wamemweka katika
jamii na kumwonyesha anavyothamini amali za jamii yake. Amali hizo ni za kidini
au kiimani, kimaarifa na kimatendo. Aidha, utafiti umebaini kuwa uandishi wao
umejiegemeza katika mikondo ya Falsafa ya Kiafrika ya kiethinofilosofia na
kihekima kama ilivyoasisiwa na Placid Tempels na Odera Oruka kwa kufuatana.
Kwa jumla, maarifa au epistemolojia ya Kibantu yameonekana yakiegemea ontolojia
kwa kila kipengele; na hivyo, kani-uhai kuonekana kama mhimili mkuu wa falsafa
ya Kibantu.
Utafiti ulioizaa tasnifu hii umeonekana kuwa na mchango mkubwa katika eneo la
Falsafa ya Kiafrika na ya Kibantu. Kwa maoni na upeo wa mtafiti, yumkini, hii ni
Tasnifu ya kwanza nchini Tanzania ya kiwango cha shahada ya uzamivu,
iliyochokoza taaluma ya Fasihi kwa mtazamo wa falsafa ya Kibantu kwa kutumia
riwaya za Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi. Vilevile, ni ya kwanza kuutumia
mkabala wa epistemolojia ya Kibantu katika uchanganuzi wa kazi za Fasihi.
Nadharia hii mpya iliyoegemea uchambuzi wa fikra za Wabantu inaweza kutumiwa
na watafiti wengine. Hali hii itasaidia kutotumia nadharia za kigeni pekee katika
kuchunguza fasihi ya Kiswahili, hata kwa mambo yasiyohusiana na mitazamo ya
kigeni. |
|