Tasnifu (MA Kiswahili)
Tasnifu hii inahusu Uwili katika Tamthiliya za Kiswahili kwa kuangalia Tamthiliya
teule za Penina Muhando. Malengo ya utafiti huu yalikuwa ni kuchambua tamthiliya
teule za Penina Muhando ili kubainisha matumizi ya uwili katika tamthiliya hizo,
kueleza sababu zilizomfanya Penina Muhando kutumia mbinu za uwili katika utunzi
wa tamthiliya teule, kadhalika kueleza dhima ya uwili katika tamthiliya teule za
Penina Muhando. Katika utafiti huu, data zilikusanywa uwandani na maktabani.
Baada ya hapo mtafiti alitumia mkabala wa maelezo katika kuchanganua data huku
akiongozwa na nadharia ya Ujumi Mweusi.
Utafiti huu ulibaini kuwa katika tamthiliya teule za Penina Muhando kuna uwili,
yaani tamthiliya zimetungwa kwa kutumia mbinu za ki-Aristotle zilizochanganywa
na mbinu za jadi za fasihi simulizi. Mbinu za ki-Aristotle ni kama ifuatavyo: msuko,
wahusika, maudhui, matumizi ya lugha, muziki na mwonekano ilhali mbinu za jadi
za fasihi simulizi ni: utambaji wa hadithi, matambiko, vitendawili, methali, nyimbo,
ngonjera na majigambo. Aidha, mtafiti alibaini sababu zalizomfanya Penina
Muhando kutumia mbinu za uwili ni kama ifuatavyo: ukombozi wa kisanaa,
kutangaza utamaduni wa ki-Afrika na Afrika kwa jumla, na ubunifu. Pia, mtafiti
alieleza dhima ya uwili katika tamthiliya teule kama ifutavyo: kuhuisha utamaduni,
kuhifadhi historia, mila na desturi, kuhimiza ushirikiano na uhuru wa msanii. Utafiti
huu ni changamoto kwa watunzi wa kazi za sanaa katika kuleta mapinduzi ya
kimtindo kwa kuingiza mbinu za jadi za ki-Afrika ikiwemo matumizi ya fasihi
simulizi iliyokuwa imesahaulika kwa muda mrefu kutokana na athari za wakoloni.