Tasnifu (Shahada ya Uzamivu katika Kiswahili)
Tasnifu hii inahusu Matumizi ya Ramsa na Tanzia katika Utenzi wa Al-Inkishafi. Tasnifu hii imelenga kuchunguza matumizi ya ramsa na tanzia, kupitia vijenzi vya kifani, matukio, sababu na kutathmini ustadi wa matumizi ya dhana hizo za ramsa na tanzia katika Utenzi wa Al-Inkishafi (1720-1820) jinsi unavyolingana na kutafautiana.
Mbinu za tasnifu zimejikita katika kushughulikia maeneo yaliyofanyika utafiti yakiwa ni maktabani na maskanini katika kisiwa cha Pate nchini Kenya. Njia zilizotumika kukusanyia data ni usaili, udurusu wa maktabani, na ushuhuda wa maskanini. Uthabiti wa data pamoja na matumizi ya mkabala wa kifasili yalihusishwa na misingi ya nadharia ya Uamilifu katika kuchambua data na kuleta tija iliyotarajiwa. Hatimaye, tasnifu imebainisha namna ilivyofuata maadili ya utafiti.
Utafiti wa ramsa na tanzia katika Utenzi wa Al-Inkishafi umegundua kwamba mshairi alikuwa na sababu maalumu za kutumia dhana hizo kinzani za ramsa na tanzia, zilizomsukuma kutumia vijenzi maalumu katika matukio kadhaa, yaliyotumika katika ustadi wa kufanana na kutafautiana. Hivyo, tasnifu hii ni muhimu katika taaluma ya tenzi za Kiswahili katika kuzipanua kimawanda dhana za ramsa na tanzia kutoka katika uwanja wa tamthiliya kuelekea katika uga wa ushairi wa Kiswahili kupitia Utenzi wa Al-Inkishafi. Hivyo, wahakiki na wachambuzi wa ushairi, kuanzia sasa nawashauri kuzijumuisha dhana za ramsa na tanzia katika uhakiki na uchambuzi wao, kwa yatayohusiana na haya.