dc.description |
Tasnifu hii ni zao la utafiti uliofanywa unaohusu Falsafa ya Waafrika na Mchango Wake katika Ujenzi wa Mtindo wa Uhalisiajabu katika Riwaya ya Kiswahili. Utafiti uliozalisha tasnifu hii umetokana na changamoto kubwa kuwa upo ugumu wa uelewekaji wa maudhui ndani ya kazi za Fasihi zinazotumia mtindo wa uhalisiajabu. Ili kutimiza azma ya kufanyika kwa utafiti huu, malengo manne yalishughulikiwa. Nayo ni kubainisha namna Falsafa ya Waafrika ilivyosawiriwa katika riwaya teule za Kiswahili za kihalisiajabu, kujadili namna Falsafa hiyo inavyojitokeza kama kijenzi cha mtindo wa uhalisiajabu katika riwaya teule za Kiswahili za kihalisiajabu, kuainisha mtindo ya uhalisiajabu kwa kuzingatia namna unavyojitokeza katika riwaya teule za Kiswahili za kihalisiajabu, na kufafanua mchango wa mtindo wa uhalisiajabu katika maendeleo ya riwaya ya Kiswahili. Njia zilizotumika kupata data za utafiti uliozalisha tasnifu hii ni usaili, udodosaji, udurusu wa nyaraka na ushuhudiaji. Data za utafiti huu zilitafsiriwa na kuchambuliwa kwa kutumia nadharia tete ya Uhalisiajabu. Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa kusawiriwa kwa Falsafa ya Waafrika katika riwaya za Kiswahili kuna mchango mkubwa katika kuujenga mtindo wa uhalisiajabu. Aidha, imebainika pia kuwa kuna aina mbalimbali za mtindo wa uhalisiajabu katika riwaya za Kiswahili za kihalisiajabu. Nazo ni: uhalisiajabu fantasia, tarazi, fifi, wa kimajazi, na wa kisitiari. Kwa upande mwingine, matokeo ya utafiti yameonesha kuwa mtindo wa uhalisiajabu una mchango mkubwa katika maendeleo ya riwaya ya Kiswahili, kifasihi na kijamii. Kifasihi, mtindo huu umechangia katika maendeleo ya riwaya ya Kiswahili kiepistemolojia, kiujumi, na katika upanuzi wa uhuru wa waandishi katika kuandika kazi zao. Kijamii, mtindo huu umeifanya riwaya ya Kiswahili kuwa ni darasa la kujifunza maarifa ya Falsafa ya Waafrika; na pia, kama ghala la kuhifadhia amali za Waafrika.
Utafiti umehitimishwa kwa kupendekeza mambo makuu mawili yafuatayo: Mosi, Serikali kuweka mikakati mathubuti ya kuhakikisha kuwa lugha na Fasihi ya Kiswahili vinapewa kipaumbele katika muktadha wa elimu na jamii kwa jumla. Pili, Usomaji wa kazi za Fasihi ufanywe kwa umakini kwa kuzingatia nadharia za uhakiki zinazoendana na kazi husika na muktadha wa jamii. |
|