Tasnifu (Shahada ya Uzamili ya Sayansi za Jamii katika
Fasihi ya Kiswahili)
Tasnifu hii inajikita katika kubainisha vipengele vya falsafa ya Kiafrika vinavyojitokeza katika riwaya ya Dunia Uwanja wa Fujo na tamthiliya ya Ngoma ya Ng’wanamalundi na kulinganisha namna Euphrase Kezilahabi na Emanuel Mbogo wanavyotumia vipengele vya falsafa ya Kiafrika katika kusuka simulizi na kuumba wahusika. Kwa kiasi kikubwa, utafiti huu ulifanyika maktabani. Kwa kiasi kidogo ulihusisha utafiti wa uwandani. Kwa mintarafu hiyo, mbinu na njia za kukusanyia data zilizotumika katika utafiti huu ni udurusu wa maandiko na mahojiano. Data tulizichambua kwa kuzingatia nadharia ya Sosholojia. Hii ni kutokana kwamba, wanasosholojia wanaamini kwamba Fasihi haiwezi kujitenga na jamii ambayo Fasihi hiyo imetengenezwa kutoka kwenye jamii hiyo. Bali hutokana na historia ya watu, utamaduni, yaani mila na desturi, uchumi na siasa ya jamii husika. Utafiti huu uligundua kuwa kazi teule zilizochunguzwa zinasawiri kwa kiasi kikubwa falsafa ya Kiafrika. Maisha ya Waafrika yamefichwa katika Fashi. Imebainika kuwa waandishi huandika kazi ya fasihi kwa kuisawiri falsafa ya jamii husika. Pia imebainika kuwa kuna kufanana na kutofautiana kwa waandishi teule katika kuvitumia vipengele vya falsafa ya Kiafrika katika kusuka simulizi na kuumba wahusika. Zaidi, utafiti ulibaini kuwa Kezilahabi ametumia vipengele vifuatavyo vya falsafa ya Kiafrika: Ulozi na ushirikina, hekima na busara, umoja, maadili, uongozi, imani na dini, dhana ya kifo na uhai, uzuri, wakati na magonjwa. Mwandishi Mbogo ametumia vipengele vifuatavyo: Ulozi na ushirikina, dhana ya kifo na uhai, uongozi na maadili. Mchango mpya ulioibuliwa kutokana na utafiti huu ni: Mosi, kubainishwa kwa vipengele vya falsafa ya Kiafrika kama vilivyojitokeza katika vitabu teule. Vipengele vitakavyosaidia jamii kujitambua zaidi kama Waafrika. Pili, Kufafanuliwa kwa namna vipengele vya falsafa ya Kiafrika vinavyoweza kutumika katika kusuka simulizi na kuumba wahusika katika riwaya na tamthiliya. Tatu, kufafanuliwa kwa nadharia ya Sosholojia pamoja na misingi yake muhimu na inavyoweza kutumika katika uchambuzi wa maswala ya falsafa ya Kiafrika.