Tasnifu (Shahada ya Kiswahili)
Utafiti huu ulilenga kuchunguza Ujumi wa Mtindo katika Mashairi Teule ya Bwana Haji Gora Haji. Utafiti huu uliongozwa na malengo matatu, nayo ni: Kuanisha mitindo iliyotumika katika kazi teule za Haji Gora. Kuchambua ujumi wa kimtindo uliotumika katika kazi teule za Haji Gora, na kutathmini ujumi wa kimtindo uliotumika katika kazi teule za Haji Gora.
Mbinu zilizotumika katika ukusanyaji wa data ni udurusu wa maktaba, usaili na mahojiano ili kupata taarifa juu ya ujumi wa kimtindo uliotumika katika kazi za Haji Gora, ikiwa ni pamoja na kutatua tatizo la utafiti kwa jumla. Nadharia iliyotumika katika utafiti huu wakati wa ukusanyaji na uchambuzi wa data ni Ujumi mweusi ambao uliongoza uchambuzi wa data za utafiti huu kupitia misingi yake.
Matokeo ya jumla ya utafiti huu, yalionesha mitindo iliyotumika pamoja na ujumi wake. Nayo ni: utumiaji wa mafumbo, taswira, matumizi ya lahaja, matumizi ya masimulizi, pamoja na mitindo mingine. Katika ujumi wa kimtindo utafiti ulibaini kuwa kazi hizi zimetumia vizuri lugha ya Kiswahili kama lugha ya Kiafrika, kuzungumzia imani na itikadi za Kiafrika, kuzungumzia mambo ya kiasili ya Kiafrika, pamoja na kuzungumzia utamaduni na historia ya Zanzibar. Pia, utafiti umetathmini na kubaini kuwa mafumbo, taswira, tamathali za semi na mitindo mingine katika kazi hizi zimesawiri vema idili na utamaduni wa jamii ya Zanzibar.