Tasnifu (Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili)
Tasnifu hii inahusu nafasi ya mwanamke katika methali za Kikerewe. Malengo ya
utafiti huu yalikuwa ni kuchunguza nafasi ya mwanamke katika methali za Kikerewe
ambazo hutumiwa katika shughuli zao za kifamilia. Data zilikusanywa uwandani na
maktabani. Baada ya hapo, mtafiti alitumia mkabala wa maelezo, pamoja na
nadharia ya Ufeministi katika kuchanganua data.
Tasnifu hii imekusudia kuziba pengo linayojitokeza kwa kuchunguza nafasi ya
mwanamke katika methali za Kikerewe. Kuweza kuzamia hasa katika matumizi ya
methali hizo kwa mwanamke, namna methali hizo zinavyomchora mwanamke na
hata pia athari za methali hizo kwa jamii.
Udodosaji na mahojiano ni mbinu zilizotumika katika ukusanyaji wa data
zilizosaidia upatikanaji wa tasnifu hii.
Utafiti huu ulibaini kuwa katika methali za Kikerewe zilizo nyingi, nafasi ya
mwanamke kwa jamii hiyo ni ya kumdunisha. Hii ni kutokana na mfumo mzima wa
maisha, mila, na desturi ambazo zimewakuza na ambazo ndicho kigezo kikubwa
kinachowafanya watumie methali katika kumshambulia mwanamke na kuamini
kuwa mwanamke ndiye chanzo cha matatizo ya kila jambo baya. Pia, tasnifu
imeeleza nafasi ya mwanamke katika methali za Kikerewe kwa kujiegemeza katika
methali kwa kumwangalia mwanamke, usawiri wa mwanamke katika methali na
athari ya methali hizo kwa mwanamke. Mchango mpya wa tasnifu hii ni kwamba,
elimu ni muhimu kwa mwanamke asiyetambua haki yake hasa kwa wale waishio
vijijini.