Tasnifu (Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili)
Utafiti huu ulilenga kuchunguza Athari za Teknolojia katika Ngano, ambao
uliongozwa na malengo matatu nayo ni kuchunguza historia ya ngano Zanzibar,
kuchambua maendeleo ya teknolojia ambayo yanaathiri ngano na kubainisha athari
za maendeleo ya teknolojia katika hadithi za ngano.
Mbinu zilizotumika ili kuweza kutatua tatizo la utafiti ni udurusu wa kimaktaba,
usikilizaji wa vyombo vya habari, mahojiano na mjadala wa vikundi. Sampuli ya
watafitiwa ilikuwa ni wanafunzi, walimu kutoka SUZA, wakaazi wa mkoa wa Mjini
Magharibi na wafanyakazi wa ZBC. Nadharia aliyotumia mtafiti katika uchambuzi
wa data ni nadharia ya uhalisia ambayo ndiyo iliyomuongoza katika uchambuzi wa
data.
Matokeo yautafiti yanaonesha kuwa chimbuko la ngano ni kuwaasa watoto juu ya
tabia ambazo hazikubaliki katika jamii, watu kujionesha kuwa wana vipawa vya
kutumia lugha na pia ni watu kutaka kujionesha namna wanavyoyaelewa mazingira
yao. Ngano ziliwasilishwa kwa mdomo. Maendeleo ya teknolojia ambayo
yanatumika kuwasilishia, kuhifadhia, kusambaza ngano ni maandishi, CD, kanda za
video na kanda za kunasia sauti pamoja na kompiyuta. Athari zinazopatikana kwa
kutumia vifaa vya teknolojia katika kuwasilisha, kuhifahia na kusambazia ngano
zimebainika kuwa zipo chanya na hasi.
Mwishowe utafiti huu umetoa mapendekezo kuwa serikali kupitia wizara husika
kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa ngano na pia kuzikusanya kwa ajili ya
kuzihifadhi ili zisipotee moja kwa moja, teknolojia ambayo itatumika kuhifadhia
ngano hizo iwe ni ya kudumu na kuigizwa ili zipate uasili wake na pia maskulini
sisitumike kufundishia lugha tu bali iwe ni nyenzo ya wanafunzi kuvuna taaluma
iliyomo katika ngano hizo.