Tasnifu (Shahada ya Uzamili ya Sayansi Jamii katika Fasihi ya Kiswahili)
Utafiti uliozaa tasnifu hii ulilenga kuchunguza matumizi ya motifu ya nambari katika ngano za Ki-Pemba. Motifu ni miegamo ambayo fanani wa kazi za fasihi huiegemea katika kujenga vipengele muhimu vya kazi zao. Nambari ni dhana inayodokeza idadi ya dhana mbalimbali kama vile watu na vitu. Motifu ya nambari hujengwa na nambari zinazotajwa kwa namna ya kurudiwarudiwa mara kwa mara na fanani wakati wa utambaji wa ngano hizo mbele ya hadhira, hivyo kuibua dhana ya motifu.
Utafiti huu ulitumia mbinu za udurusu wa kimaktaba, usaili, ushuhudiaji pamoja na mjadala wa vikundi lengwa katika kukusanya data. Data za kimaktaba zilikusanywa katika miji ya Dodoma, Dar-es-Salaam na kisiwani Unguja. Data za uwandani zilikusanywa visiwani Zanzibar yaani Unguja na Pemba. Nadharia iliyotumika katika kutafiti na kuchambua data za utafiti ni ya uhalisia. Kadhalika, utafiti ulichukua sura ya ufafanuzi wa kimaelezo katika mchakato mzima wa utafiti.
Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa matumizi ya motifu ya nambari yana dhima kubwa kwa upande wa Fasihi, hususan Fasihi Simulizi, na kwa jamii husika. Uchunguzi umeonesha kuwa kuna kuoana kwa kiasi kikubwa baina ya miktadha mbalimbali ya jamii za Wapemba ambayo huhusisha matumizi ya nambari na jinsi inavyojitokeza katika ngano zao. Miktadha hiyo ni ya kidini, kiutamaduni, kiujumi, kijografia, kihistoria na kiisimu. Yote hii hufungamana na matumizi makubwa ya nambari katika uendeshaji wa vipengele mbalimbali vinavyopatikana katika maisha. Vipengele hivyo ni kama vile mikusanyiko ya harusi na matanga, tiba za asili, ndoa na uzazi, shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji sanaa pamoja na kazi za amali zihusuzo jamii husika. Dhima za nambari katika ngano za Ki-Pemba zilizoibuliwa na utafiti ni kudhihirisha ujaala, ujadi, kutamblisha ujumi wa Wapemba na kuzipamba ngano zenyewe.
Mchango mpya ulioibuliwa na tasnifu hii ni kupambanuliwa kwa dhana ya motifu ya nambari pamoja na kubainishwa kwa mdhihiriko na matumizi yake katika kazi za fasihi. Kwa maoni ya mtafiti, hili ni miongoni mwa maandiko machache yanayopambanua dhana hii ya motifu ya nambari katika fasihi ya Kiswahili.