dc.description |
Utafiti huu umehusisha taswira katika Fungate ya Uhuru na Wasakatonge.
Chimbuko la tatizo limetokana na hali ya kila siku ya utumiaji na uelewaji mdogo
wa taswira kwa wasomaji na wasikilizaji katika kazi mbalimbali za ushairi. Hivyo
utafiti huu umejikita kuchunguza taswira katika diwani za Fungate ya Uhuru na
Wasakatonge. Pia utafiti huu umekuwa na malengo mahsusi matatu ambayo ni
kuzichambua taswira zilizojitokeza katika diwani teule za mashairi ya Khatib, Aidha
kuchunguza sababu za Khatib kutumia taswira katika diwani teule hizi na kubainisha
matokeo ya matumizi ya taswira katika diwani za mashairi ya Khatib kwa wasomaji.
Taarifa za utafiti huu zilikusanywa kwa njia ya mahojiano, majadiliano, madodoso
na mapitio ya maandishi. Sampuli hizo zimegawa katika makundi mawili ambayo ni
walimu wanao fundisha somo la Fasihi na wanafunzi wanaosoma somo hilo kwa
kidato cha nne na kidato cha sita katika shule ya sekondari Ilolo na Vwawa.
Uchunguzi wa taarifa za utafiti zilizokusanywa zimeongozwa na nadharia ya
mwitikio wa msomaji ambapo uchambuzi ulifanyika kwa mbinu ya ufafanuzi.
Matokeo ya utafiti huu yameonesha kwamba diwani za Fungate ya Uhuru na
Wasakatonge zina taswira nyingi ambazo zimejitokeza sehemu mbalimbali za
diwani hizi. Taswira hizo zilizojitokeza ni zile za baadhi ya makundi ya kibayolojia,
kiteolojia, na taswira za kawaida. Matokeo ya utafiti huu yamebainisha sababu
mbalimbali za mwandishi Khatib kutumia taswira katika diwani teule. Sababu hizo
ni pamoja na kuficha au kupunguza ukali wa maneno, kuwasilisha dhana moja kwa
wakati mmoja na kuzileta hisia na fikra za wasomaji. Hata hivyo, utafiti huu
umebainisha matokeo chanya na hasi ya matumizi ya taswira kama vile kupanua
fikra za wasomaji na utata katika kupata maudhui yaliyokusudiwa. Mwisho utafiti
huu umeonesha muhtasari wa utafiti, mapendekezo ya utafiti, matokeo ya utafiti,
changamoto za utafiti na mambo mapya yaliojitokeza katika utafiti huu. |
|