Tasnifu (Shahada ya Uzamili ya Sayansi Jamii katika Fasihi ya Kiswahili)
Utafiti huu ulijadili kuhusu Taswira ya mwanamke katika Muziki wa Nyimbo za
Dansi teule za Mbaraka Mwinshehe. Tatizo lililojenga utafiti huu ni kutokana na hali
ya kila siku iliyopo kwa wasanii wa muziki wa nyimbo za dansi, wakiwemo wanaume,
kumkweza mwanaume kinafasi na kimajukumu na kumtweza mwanamke.
Utafiti ulitumia mbinu ya maktabani kwa kuchunguza kazi mbalimbali zilizoandikwa
kuhusu usawiri wa mwanamke na mgawanyo wa majukumu kijinsia. Pia, nyimbo teule
za Mbaraka Mwinshehe zimesikilizwa kwa makini ili kuweza kujua ni jinsi gani
mwanamke amechorwa. Pia, mahojiano yalifanyika ili kuweza kupata na kuelewa kwa
undani mada ya utafiti. Nadharia iliyoongoza utafiti huu ni ya Ufeministi, hususani wa
Kiafrika, ambao una mawazo yanayozungumzia harakati za kumkomboa mwanamke
katika jamii inayomdharau na kumkandamiza. Utafiti umebaini kuwa kuna tofauti
kubwa za kimajukumu kati ya mwanamume na mwanamke katika jamii. Kwa asilimia
kubwa, mwanamke amechorwa kwa upande hasi, yaani mnyonge, tegemezi na kiumbe
duni. Hali imefanya mwanamke azidi kudharaulika, kutothaminiwa na kukejeliwa.
Kwa kiasi kidogo, amechorwa ni mtu muhimu katika familia, hususani katika suala la
kumstarehesha mwanaume awapo na shida. Vile vile, utafiti umebaini kuwa kuna
athari kubwa kwa jamii zinazosababishwa na usawiri wa mwanamke katika nyimbo za
dansi. Athari mojawapo ni kwa wasomaji kuiga matendo mabaya ambacho ni chanzo
cha mwanamke kuendelea kudharaulika na kutothaminika katika jamii. Athari
nyingine ni kuiga yale mema yanayompa hamasa mwanamke kuendelea kujituma
katika majukumu mbalimbali.
Hitimisho la Tasnifu hii ni kwamba mwanamke amekuwa ni mtu wa kutwezwa wakati
huo mwanaume anakwezwa. Yote hayo yanasababishwa na mila na tamaduni mbovu
zilizopo katika jamii ambazo zinamchukulia mwanamke kama kiumbe kisichoweza
wakati wote na kuwa kinahitaji msaada kila wakati. Hata hivyo, utafiti umebaini kuwa
ukweli hauko hivyo, mwanamke anaweza kuleta maendeleo bila utegemezi.