Tasinifu (Shahada ya Uzamili Sayansi ya jamii katika Fasihi ya Kiswahili)
Utafiti huu ulichunguza utani katika sherehe za harusi za Watumbatu. Utani ni chombo
muhimu kinachowasilisha fikira, ujumbe na mwelekeo wa kijamii. Kwa kutumia utani
jamii hutambulisha asili, utamaduni wake pamoja na kurithisha mila na silka za jamii.
Watani hutupiana maneno yenye mzaha, kejeli, izara na hata matusi makali bila
kuzingatia wale wanaowasikiliza, jambo ambalo baadhi ya hadhira hulalamikia jambo
hilo.
Utafiti huu ulifanyika katika kisiwa cha Tumbatu chenye shehia tatu ambazo ni Uvivini,
Jongowe na Gomani. Watafitiwa walikuwa hamsini na watano (55).Mbinu zilizotumika
katika utafiti huu ni udurusu, mahojiano, udodoshaji na ushuhudiaji. Nadharia
iliyoongoza utafiti huu ni ya Uhemenitiki ambayo inaongozwa na msingi wa kufasiri
matini kwa kuzingatia utukuzaji na ufufuaji wa maana za matini kimuktadha, kisaikolojia
na kisarufi. Hivyo taashira zilizomo ndani ya utani ziligunduliwa kupitia misingi ya
nadharia hii.
Matokeo ya utafiti yameonesha kuwapo kwa aina nne za utani ufanyikao katika
sherehe za Watumbatu. Nazo ni utani wa binamu, utani wa mashemeji, utani wa babu/
bibi na wajukuu, na utani wa marafiki. Utani huo hufanywa kwa sababu ya
kujitambulisha, kuonesha mahusiano, kufunza na kuburudisha. Aghalabu, utani huo
ufanyikao katika sherehe za harusi hutamalakiwa na matumizi ya matusi na kejeli
ambazo huwa na taashira maalumu iliyokusudiwa.Pia, utafiti uligundua na kubainisha
taashira mbalimbali zinazotokana na utani kupitia maneno na matendo. Hii ni kwa
sababu hutoa ujumbe maalumu unaopaswa kuzingatiwa na wanandoa na hata hadhira
shiriki wa harusi hiyo. Hii ina maana kuwa utani una nafasi muhimu katika jamii.