Description:
USANIFISHAJI WA KISWAHILI AFRIKA MASHARIKI, CHANGAMOTO NA NAMNA YA KUKABILIANA NAZO.
Mussa M. Hans –mussahans30@gmail.com
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili- Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Ikisiri
Mchakato wa usanifishaji wa lugha ya Kiswahili ulianza siku nyingi, hata kabla nchi za Afrika Mashariki hazijapata uhuru. Baada ya nchi hizi kupata uhuru bado mchakato huo umeendelea japo kwa malengo na mbinu tofauti. Wakati tukiwa tunajadili kuhusu mchakato wa usanifishaji wa lugha ya Kiswahili katika nchi za Afrika Mashariki, ni vema tukatilia maanani kuhusu mfumuko wa istilahi, hasa istilahi zinazohusu maendeleo ya sayansi na teknolojia ambazo huibuka kila uchao. Aidha, tukumbuke pia kwamba hivi sasa kuna mfumuko wa vyuo vikuu na Kiswahili ni miongoni mwa masomo yanayosomwa na wanafunzi wengi katika vyuo hivyo. Wanafunzi hao kwa yakini wanahitaji vitabu vya kutosha vya marejeo tena vilivyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Wanajumuiya hawa pia wanahitaji kuwa na istilahi kubalifu katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja istilahi za utafiti hasa ukitilia maanani kwamba lugha ya mawasiliano katika ufundishaji wa somo hili ni Kiswahili. Katika mazingira kama haya kuna umuhimu wa kusimamia kwa makini mchakato wa usanifishaji wa istilahi za Kiswahili katika nyanja mbalimbali ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo la makala haya ni kujadili changamoto zinazolikabili zoezi la usanifishaji wa Kiswahili katika jumuiya mpya ya Afrika Mashariki. Makala haya pia yatatoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kuwa na matumizi bora ya lugha ya Kiswahili miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Maneno ya msingi: usanifishaji, Afrika mashariki na changamoto, Kiswahili