Tasnifu (Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili)
Utafiti huu ulilenga kuchunguza mabadiliko ya kasida katika dhima na uwasilishaji
wake Zanzibar ambao ulifanyika katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa ni kuchunguza mabadiliko ya kasida katika jamii
ya Zanzibar katika dhima na uwasilishaji wake. Malengo mahsusi yalikuwa ni
kutambulisha mabadiliko ya dhima yaliyojitokeza katika kasida za Kiswahili
zinazotumiwa na jamii ya watu wa Zanzibar, kubainisha mabadiliko katika
uwasilishaji wa kasida za Kiswahili zinazotumiwa na jamii ya Zanzibar pamoja na
kuona athari za mabadiliko hayo. Mtafiti alitumia utaratibu wa uwandani na wa
maktabani ambao ulitumia njia ya upekuzi wa marejeleo, uchunguzi shirikishi
pamoja na usaili. Jumla ya kasida ishirini zilizilifanyiwa utafiti wa kina pamja na
watafitiwa hamsini wakiwemo wazazi, walimu pamoja na wanafunzi wa madrasa.
Nadharia ya Ubadilikaji Taratibu ndiyo iliyomuongoza mtafiti katika uchanganuzi
wa data hizo zilizoteuliwa.
Utafiti umeonesha kuwa yapo mabadiliko mbali mbali ya kasida katika uwasilishaji
wa kasida pamoja na maudhui ya kasida katika jamii ya Wazanzibari na kwamba
kasida husomwa kulingana na muktadha au matukio mbali mbali yanayojitokeza
katika jamii husika. Pia utafiti uligundua kwamba kasida za Kiswahili zina nafasi
nzuri katika kujenga maadili ya jamii husika kwani zimejikita karibu katika kila
nyanja ya maisha ya Mzanzibari. Utafiti huu umeshauri jamii pamoja na wadau
mbali mbali kuendeleza na kulinda hadhi ya kasida ili kuweza kutunza maadili ya
jamii ya watu wa Zanzibar.