Tasnifu (Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili)
Utafiti huu ulihusu taswira zinazojitokeza katika ngano za Kiswahili. Utafiti huu
ulifanyika katika vijiji vya Wilaya ya Kusini, Unguja.
Lengo kuu la utafiti huu nikuchambua taswira zinazojitokeza katika ngano za
Kiswahili. Malengo mahsusi yalikuwa ni kubainisha na kuchambua taswira
zinazojitokeza katika ngano za Kiswahili, kuchunguza sababu zinazoibua mitindo ya
lugha katika taswira za ngano na kuchambua uwiano wa kitaswira na kidhamira kati
ya ngano na jamii. Jumla ya ngano kumi na nne zilifanyiwa uchambuzi wa kina
pamoja na watafitiwa ishirini na nane wakiwemo wazee ambao wana tajriba kuhusu
ngano. Kwa upande wa walimu na wanafunzi walitafitwa kwa sababu wao ndio
wana uelewa mkubwa kuhusu dhana ya taswira. Katika mchakato wa ukusanyaji
data, mtafiti alitumia utaratibu wa uwandani na wa kimaktaba ambao ulitumia njia
ya upekuzi wa marejeleo, ushuhudiaji na usaili. Nadharia ya Mwitiko wa Msomaji
ilitumika wakati wa kuwasilisha na kufafanua data za utafiti huu.
Uchambuzi wa taswira za ngano za Kiswahili uliofanywa katika sura ya nne umetoa
matokeo mengi, matokeo hayo ni kama; utafiti ulibaini kuwa lugha inayotumika
katika ngano ni lugha ya kitaswira, haswa matumizi ya taswira za hisi, taswira za
kuonekana na taswira za mawazo. Pia utafiti uligundua kwamba taswira hizo zinatoa
uhuru wa kuyaeleza mambo mazito yanayoizunguka jamii ya watu wa Wilaya ya
Kusini. Halikadhalika, utafiti uliona kuwa zaidi ya taswira moja inaweza ikatumika
katika ngano moja. Utafiti huu umetoa maoni kwa Serikali ya Mapinduzi ichukuwe
juhudi za makusudi kuingiza utanzu wa ngano katika mtaala wa elimu ili ziweze
kufundishwa kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu. Wazazi nao wanajukumu la
kupata muda wa kuwasimulia ngano watoto wao ili kujenga maadili mema na iwe
hazina na urithi bora.