Tasnifu (Shahada ya Uzamili Sayansi Jamii katika Fasihi ya Kiswahili)
Tasnifu hii ilijikita katika kuchunguza nafasi ya Ukristo katika ushairi wa
Mnyampala. Mada hii haijawahi kuchunguzwa ingawa wapo waliofanya utafiti wa
kazi za mshairi huyu. Eneo la utafiti huu lilijikita katika kubainisha sababu na faida
ya Mnyampala kujielekeza katika kuandika mashairi ya dini ya Kikristo.
Asilimia kubwa ya utafiti huu ulifanyika maktabani ni kwa sababu taarifa nyingi juu
ya Mnyampala zipo katika machapisho aliyoyaandika yeye na kutoka kwa waandishi
mbalimbali. Vivyo hivyo mtafiti alikwenda uwandani kukutana na baadhi ya watu
waliokuwa karibu na mtafitiwa na waliofanya tafiti juu ya kazi zake.
Matokeo ya utafiti huu yamedhihirisha kuwa, Mnyampala ni mshairi Mkristo
aliyekomaa kiimani kutokana na mafundisho ya imani ya kanisa Katoliki.Kutokana
na kipaji chake cha ushairi, uamuzi wake wa kutumia ushairi katika kueneza Ukristo
ulifata nyayo za washairi kadha waliomtangulia ambao walitumia ushairi kueneza
imani zao. Aidha imebainika kuwa mchango wa Mnyampala kishairi umesaidia
kukuza taaluma ya ushairi kwa kuongeza maneno mapya yenye dhana ya Ukristo.