Tasnifu (Shahada ya Uzamili ya Sayansi Jamii katika Fasihi ya Kiswahili)
Tasnifu hii, inahusu Matumizi ya Utanzia katika Riwaya Teule za Said Ahmed
Mohamed. Riwaya zilizochuguzwa ni Utengano, Dunia Mti Mkavu na Kiza Katika
Nuru. Dhana ya utanzia katika tasnifu hii ina maana ya maneno matendo au
mazingira yanayozua kwa hadhira huzuni, jitimai, majonzi, masikitiko, majuto na
maumivu ya mwili, roho au akili. Utanzia unajengwa na vipengele kama vile vifo,
ajali, vifungo, mabalaa, ulemavu, vilio, maradhi, njaa na mateso. Yumkini, hakuna
uchunguzi wa kutosha kuhusu matumizi ya utanzia katika kazi za fasihi ya Kiswahili.
Hali hii imesababisha tatizo katika kuzielewa kazi mbalimbali za fasihi ya Kiswahili.
Utafiti ulifanyika maktabani na uwandani. Maktabani tuliyadurusu mapitio
mbalimbali kama vile: Majarida, tasnifu, tahakiki, makala na vitabu. Uwandani
tulitumia mbinu ya mahojiano, majadiliano na udodosi. Kwa namna fulani mbinu
hizi zilitusaidia katika kukusanya data mbalimbali zinazohusiana na utafiti huu.
Maeneo ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Kusini Unguja, Dodoma na Dares
Salaam yalitumika katika ukusanyaji wa data. Utafiti ulitumia nadharia ya Mwitiko
wa Msomaji ambayo ilitumika kwa kupata fikra binafsi za wasomaji kutokana na
uelewa wao wa vitabu teule walivyovisoma. Uchambuzi wa data uliegemea katika
maelezo kwa kuwa utafiti huu ni wa kitaamuli. Hivyo, haukujihusisha na mwegamo
wa kitakwimu.
Matokeo ya utafiti yanaonyesha utanzia ni mbinu ya kibunulizi inayofungamana na
utanzu mkongwe wa tamthiliya za kitanzia ambazo ndani yake hutoa athari maalum
kwa wasomaji.