Tasnifu (Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili)
Utafiti huu umechunguza suala la Ulinganishi wa Kidhamira wa Nyimbo za
Bongo Fleva na Hadithi Fupi za Magazeti ya Udaku, kwa kutumia nyimbo za
Bongo Fleva na hadithi fupi zilizomo ndani ya Magazeti ya Udaku. Mtafiti alipata
wazo la kufanya utafiti huu kutokana na watafiti wengi kujikita katika lugha,
matatizo yanayowakumba wanamuziki, na katika hadithi; kuchunguza athari za
dhamira, hadithi za makabila, na hadithi fupi za Kiswahili. Lakini hakuna
aliyelinganisha dhamira za muziki na hadithi. Kipengele cha ulinganishaji wa
dhamira hakikupewa kipaumbele kutokana na kujikita zaidi katika kuchunguza vitu
viwili kwa wakati mmoja. Mtafiti ameongozwa na nadharia ya Upokezi/mwitikio wa
msomaji katika kuyafikia malengo yake. Malengo ya utafiti huu yalikuwa
kulinganisha dhamira za nyimbo za Bongo Fleva na hadithi fupi za Magazeti ya
Udaku, ili kuona kama dhamira hizo zinafanana au kutofautiana katika jamii.
Matokeo ya utafiti huu yamebainisha kwamba dhamira zilizopo ndani ya Muziki wa
Bongo Fleva na hadithi fupi za Magazeti ya Udaku zinafanana, zinafanya kazi sawa
na zina lengo moja katika jamii.
Vile vile utafiti huu umeweza kuonyesha wazi, kuwa muziki wa Bongo Fleva na
hadithi fupi za Magazeti ya Udaku vina mchango mkubwa katika jamii, kwani
vinaelimisha, vinaburudisha, vinakosoa na kutoa muongozo katika jamii. Hivyo,
watu wasivipuuze na kuona ni vitu visivyofaa na visivyokuwa na thamani katika
jamii, au kuona ni vya kihuni na vinawahusu vijana tu. Bali watunzi na waandishi
wazingatie zaidi tamaduni za Kiafrika, katika kuimba na kuandika kazi zao, pia
katika uchapishaji wa magazeti hayo ya udaku na uvaaji wa wanamuziki vijana.