Tasnifu (Shahada ya Uzamili ya Fasihi ya Kiswahili)
Tasnifu hii ni matokeo ya utafiti uliojikita katika kufanya uchambuzi wa vipengele
vya kiujumi katika Fasihi simulizi, hususani katika hotuba teule za Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere. Madhumuni ya tasnifu hii ni kuweka wazi vipengele vya
kiujumi vilivyomo katika hotuba hizo ili kuonesha uthibitisho kuwa taaluma ya
ujumi inayo nafasi kubwa katika Fasihi simulizi. Pia tumefanya uchambuzi ili
kuweza kuwianisha vipengele vya ujumi vinavyopatikana katika hotuba hizo na hali
halisi ya maisha ya Watanzania, pamoja na kubainisha athari za kiujumi. Utafiti huu
ulifanyika maktabani na uwandani ulitumia mbinu ya uchambuzi wa matini, pamoja
na mahojiano. Uchambuzi wa data ulifanyika kwa njia ya ufafanuzi na data
tulizozipata ziliwasilishwa kwa njia ya maelezo. Aidha, vielelezo vilitumika. Utafiti
huu ulimakinikiwa na kuongozwa na mkabala wa Ki- Marx ambao ni mkabala
unaotumia mbinu za kiupembuzi katika kuchanganua mambo ya kijamii na
kiutamaduni. Kwa jumla, ili kumakinika vema katika masuala ya kiujumi, hatuna
budi kuwa na utambuzi wa idili za jamii husika. Tasnifu hii ina jumla ya sura tano.
Sura ya kwanza imeeleza usuli wa mada, tamko la utafiti, malengo ya utafiti,
maswali ya utafiti, umuhimu wa utafiti, na mawanda ya utafiti. Sura ya pili imeeleza
mapitio ya maandiko yanayohusu ujumi na hotuba, pamoja na mapengo
yaliyojitokeza. Sura ya tatu ya mchakato huu tumeeleza mbinu za utafiti, eneo la
utafiti na vifaa vya utafiti, pamoja na mkabala wa utafiti. Njia zilizotumika katika
kukusanya data ni mbinu ya uchambuzi wa matini, pamoja na mahojiano. Sura ya
nne uwasilishaji na uchambuzi wa data. Uchambuzi kuhusiana na masuala ya
kiujumi katika hotuba hizo. Sura ya tano ambayo ndiyo sura ya mwisho kwa mujibu
wa tasnifu hii, inahusu hitimisho na mapendekezo.