Ikisiri. Makala kamili inapatikana http://journals.unam.edu.na/index.php/JULACE/article/view/1476
Makala haya yanakusudia kuchunguza namna uforensiki unavyoibua ujumi wa riwaya pendwa ya Kiswahili, sambamba na kuitambulisha taaluma ya uforensiki inavyojitokeza katika riwaya ya Kikosi cha Kisasi. Kutofahamikavyema kwa taaluma ya uforensiki katika riwaya pendwa ya Kiswahili, kumesababisha mtazamo hasi kwa wadau mbalimbali wa fasihi ya Kiswahili kama vile Kimura (1991), Hussein (1971) na Kezilahabi (1976), waliotafiti na kuihakiki riwaya pendwa ya Kiswahili na kuiona kuwa ni riwaya isiyo na mafunzo yenye maadili kwa jamii, kutokana na maudhui yake ya ujambazi, mauaji, uhalifu, ujasusi, mapenzi na upelelezi kuelezwa waziwazi. Hali hii imesababishwa na uchache wa wanataaluma waliojihusisha na tafiti zinazohusu uforensiki katika riwaya pendwa ya Kiswahili. Hata hivyo, suala la uforensiki katika kuibua ujumi wa riwaya pendwa ya Kiswahili halijashughulikiwa. Kutoshughulikiwa huko kunaendeleza mtazamo hasi wa kuziona riwaya hizi kuwa zimeiga utamaduni wa kigeni na hazina umuhimu katika jamii yetu, licha ya kuwa jamii yenyewe tayari imeshaathiriwa na utandawazi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia.. Makala haya yatasaidia kuondoa mtazamo hasi uliopo juu ya riwaya pendwa ya Kiswahili na kuidhihiridha namna uforensiki unavyoibua ujumi katika riwaya pendwa ya Kiswahili hususani riwaya ya Kikosi cha Kisasi.