Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili
Tasnifu hii inajadili suala la ufungwa katika diwani za Sauti ya Dhiki (1973) na
Chembe cha Moyo (1988). Tatizo lililomsukuma mtafiti kufanya utafiti huu ni kwa
kuwa tafiti katika uga huu wa ufungwa bado ni finyu. Kwa kutumia nadharia ya
uhemenitiki na nadharia ya Ki-Marx mtafiti alichunguza suala la ufungwa katika
ushairi wa Kiswahili kwa kutumia diwani teule.
Data zilikusanywa maktabani na uwandani maeneo ya Zanzibar, Kenya, Dar es
Salaam na Dodoma. Mbinu zilizotumika katika utafiti huu ni udurusu wa
maktabani, njia ya udodosaji na njia ya mahojiano. Data zilichanganuliwa kwa
kuzingatia njia ya maelezo ya utafiti pamoja na misingi ya nadharia za Uhemenitiki
na Ki-Marx.
Utafiti umegundua namna ufungwa ulivyokabiliwa na vikwazo vikubwa katika jamii
inayohusiana na wafungwa. Kwa hivyo, utafiti umetoa mchango mkubwa kuhusiana
na suala la ufungwa katika kipengele cha fasihi andishi ya Kiswahili kwa upande wa
ushairi. Mchango mpya ulioibuliwa kutokana na utafiti ni huu ufuatao: Utafiti
umegundua matatizo yanayowapata wafungwa wa aina yoyote katika jamii, kwa
mfano, ufungwa wa gerezani, mfungwa anapowekwa gerezani huteswa na hukatiwa
matumaini yake yote katika mustakbali wa maisha yake. Pia, kumpotezea malengo
kwa watu waliomzunguka akiwa kama ni muhimili mkuu wa jamii hiyo ikiwemo
familia. Tatizo hili linaweza kurekebishika. Wafungwa badala kuadhibiwa vikali
magerezani wakatumiwa kama rasilimali watu kwa kutumia ujuzi walionao
kunufaisha jamii na taifa kwa jumla. Aidha, utafiti umeonesha namna ambavyo
nadharia za Uhemenitiki na Ki-Marx kwa kutumia misingi yake ilivyokuwa faafu
kwa utafiti huu.