Tasnifu (Uzamili Fasihi ya Kiswahili)
Utafiti huu ulichunguza uhalisia wa maisha ya jamii ya Wanyakyusa unavyosawiriwa katika nyimbo za ngoma ya Maghosi. Ngoma ya Maghosi ni ngoma ambayo huchezwa na jamii ya Wanyakyusa wanaoishi kwenye vijiji mbalimbali ambavyo vinapatikana katika wilaya ya Rungwe wakati wa kiangazi baada ya mavuno.
Data zilikusanywa uwandani; ambapo mtafiti alikwenda katika mazingira halisi na kutumia mbinu ya kushuhudia na mahojiano. Uchambuzi na uchanganuzi wa taarifa zote zilizopatikana katika mchakato wa utafiti uliongozwa na nadharia ya Usosholojia na kuwasilishwa kwa kutumia mbinu ya ufafanuzi.
Matokeo ya utafiti huu yanaonesha kwamba, nyimbo za ngoma ya Maghosi zimesheheni dhamira lukuki. Miongoni mwa dhamira hizo ni, uwajibikaji na kutowajibika kwa viongozi, umoja na mshikamano, unyonyaji, kuinua kipato cha wananchi, uaminifu katika ndoa, tahadhari ya magonjwa hatari, ndoa za kulazimishwa, suala la malezi, kutunza bikira na suala la mavazi. Aidha, utafiti umegundua kuwa dhamira zinazopatikana kwenye nyimbo hizo zinasawiri maisha halisi ya jamii ya Wanyakyusa kutokana na fasihi kuakisi yale yaliyotokea/yanayotokea katika jamii husika.