Tasnifu (Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili)
Utafiti huu ulichunguza dhima ya taswira katika nahau za Kisambaa, uliongozwa na
malengo matatu ambayo ni: kuchunguza namna taswira zinavyojitokeza katika
nahau za Kisambaa, kuchunguza athari zinazojitokeza katika matumizi ya taswira
katika kufafanua na uelewekaji wa nahau za Kisambaa kwa hadhira pamoja na
kutathimini uhusiano uliopo baina ya taswira zipatikanazo katika nahau za Kisambaa
na maisha halisi ya jamii.
Mapengo yaliyojitokeza katika kutoa msukumo wa kufanya utafiti huu ni haya;
Kwanza, wengi wa wataalam hao wamezishughulikia nahau kwa kuzikusanya na
kuangalia maudhui yake kama walivyotajwa katika usuli wa tatizo la utafiti, hata
hivyo, hawakukishughulikia kipengele cha taswira. Pili, uchunguzi wao umejigeza
katika nahau za Kiswahili na lugha nyingine lakini sio lugha ya Kisambaa.
Mbinu ya udodosaji, mahojiano na mjadala wa vikundi zilitumika katika kukusanya
data. Mbinu ya ufafanuzi ilitumika ambapo mkabala wa Umuundoleo ulitumika
katika uchambuzi wa data.Vitongoji vitatu pamoja na Chuo Kikuu cha Sebastian
Kolowa vilihusishwa katika kuwakilisha watafitiwa.
Matokeo ya utafiti yanabaini kuwa nahau za Kisambaa zimeenea katika vipengele
mbalimbali vya maisha ya jamii hiyo. Nahau zilizochambuliwa zinaakisi mazingira
yanayoihusu jamii hiyo pamoja na vitu vitumikavyo katika jamii husika.
Mchango mpya ambao umeibuliwa katika utafiti huu ni kukuza ufahamu juu ya
matumizi ya taswira katika Fasihi, hususani katika kipengele cha fani ambapo
taswira chomozi katika nahau za kisambaa zimeelezwa kama sehemu ya taaluma
katika Fasihi simulizi ya Kiswahili.