Tasnifu (Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili)
Lengo kuu la utafiti huu lilikuwa ni kuchunguza usawiri wa mwanamke katika
filamu za Kibongo kwa kujiegemeza katika filamu teule za Steven Kanumba.
Nadharia ya Ufeministi ndiyo iliyotumika katika uchambuzi wa data wa tasnifu hii.
Data zilikusanywa ni pamoja na filamu teule mbili za Steven Kanumba. Filamu hizo
zilitazamwa na kuchambuliwa ili kupata umaizi wa usawiri wa mwanamke. Vilevile,
makala, vitabu na tasnifu mbalimbali vilisomwa ili kuona ni kwa namna gani
mwanamke amesawiriwa.
Utafiti huu umebaini kuwa katika filamu za Kibongo, mwanamke amesawiriwa kwa
namna mbalimbali kama vile mama, mtoto, kijakazi, mwalimu, mzimu pamoja na
kahaba. Vile vile, utafiti huu umebaini kuwa jamii inamchukulia mwanamke katika
mtazamo hasi. Mtazamo huo wa jamii juu ya mwanamke ni pamoja na vipigo na
manyanyaso, kiumbe cha kustarehesha ulimwengu, malaya na muasi wa maadili,
kiumbe dhaifu pamoja na kuzalishwa na kutelekezwa.
Utafiti huu umebainisha dhamira mbalimbali zilizojitokeza kuhusu usawiri wa
mwanamke dhamira hizo zimejitokeza katika pande mbili. Kwa upande wa kwanza
dhamira hizo zimejitokeza katika hali chanya kama vile ujasiri na uvumilivu
malezi, usiri na staha kwa mwanamke pamoja na misimamo katika maisha. Pia
utafiti huu umebinisha dhamira zinazomsawiri mwanamke katika hali hasi kama vile
ukatili, unafiki na usaliti, utovu wa maadili pamoja na ushirikina. Aidha, utafiti huu
umebaini kuwa adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe.