Tasnifu (Shahada ya Uzamili katika Fasihi ya Kiswahili)
Utafiti huu ulihusu uchunguzi wa fani katika methali za Kisukuma katika uadilishaji
wa watoto na vijana. Vipengele vya kifani vilivyochunguzwa na kuchambuliwa ni
matumizi ya lugha, wahusika na mandhari. Vipengele hivyo vilichunguzwa kwa
lengo la kubainisha namna mfungamano wake unavyochangia kuibua maudhui
ambayo hukamilisha tendo zima la kiusemi na namna nguvu ya tendo kusudiwa
inavyopokewa na watoto na vijana. Nadharia ya Tendo la Kiusemi (TELAKI)
imetumika kuchanganulia vipengele hivyo. Na nadharia ya tafsiri baina ya tamaduni
mbili imetumika kwa ajili ya kutafsiri methali za Kisukuma kwa Kiswahili.
Katika utafiti huu, jamii ya watafitiwa ilikuwa ni Wasukuma waishio katika maeneo
ya mkoa wa Mwanza. Mbinu ya sampuli ya kitabaka ilitumika kuwapata watoto na
vijana na sampuli lengwa kwa wazazi na walezi kutokana na tajiriba waliyo nayo
katika matumizi ya methali. Ukusanyaji wa data ulihusisha data za uwandani na
maktabani. Data zilichanganuliwa kwa njia ya mahojiano na majadiliano baina ya
watafitiwa wa makundi yaliyolengwa na kuwasilishwa kwa njia ya ufafanuzi.
Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa maadili yaliyomo katika methali za Kisukuma
yanatokana na ufungamanifu uliopo kati ya lugha, wahusika na mandhari
iliyotumika kuijenga fani ya methali husika. Vipengele hivyo vya kifani ndivyo
hubeba matendo kusudiwa yenye ujumbe wa aina mbalimbali unaolenga kuwajengea
watoto na vijana maadili faafu katika jamii. Utafiti ulibaini pia kuwa vipengele
hivyo vya fani, kwa baadhi ya methali, hutoa changamoto kwa watoto na vijana
katika kuuelewa ujumbe uliokusudiwa.