Tasnifu (Shahada ya Uzamili ya Fasihi ya Kiswahili)
Tasnifu hii, imejikita katika kuangalia na kuchunguza mchango wa Andanenga
katika ushairi wa Kiswahili. Tasnifu hii imejielekeza zaidi katika kuangalia na
kuchunguza mchango wa kidhamira na kimuundo katika ushairi wa mwandishi huyu.
Kuna mchango mkubwa wa ushairi wa Andanenga katika ushairi wa Kiswahili,
lakini tafiti na tahakiki za kina hazijafanyika bado juu ya mshairi huyu mwenye
ulemavu wa macho. Ingawa tafiti na tahakiki nyingi zimefanywa kuhusu ushairi wa
Kiswahili na maisha ya washairi, bado tafiti na tahakiki nyingi hazijamuangalia kwa
jicho yakinifu mshairi huyu. Kutokana na hilo, mtafiti wa kazi hii aliona kuna haja
ya kufanya utafiti kwa kina zaidi ili kubaini mchango wa mwandishi huyu katika
kuendeleza ushairi wa Kiswahili hasa katika kubaini mchango wake wa kidhamira na
kimuundo katika ushairi wa Kiswahili. Lakini pia kuna haja ya kujua mbari yake na
maisha ya mshairi huyu. Asilimia kubwa ya utafiti huu ulifanyika maktabani na
udurusi wa vitabu teule vya mwandishi huyu ambavyo ni Diwani ya Ustadh (1993)
na Bahari ya Elimu ya Ushairi (2002). Kadhalika mtafiti pia alikwenda uwandani
kukutana na baadhi ya watu wa karibu wa mtafitiwa na kuhojiana na mtafitiwa
mwenyewe. Pia, baadhi ya maeneo ikiwemo TATAKI ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam ilitembelewa ili kupata taarifa zaidi. Matokeo ya utafiti huu yamedhihirisha
kuwa Andanenga ana mchango mkubwa katika ushairi wa Kiswahili kidhamira na
kimuundo. Kidhamira, yanaonekena mambo mengi yaliyojadiliwa na mshairi huyu
katika mashairi yake yanasadifu na kuhalisika katika maisha ya kila siku ya jamii ya
Watanzania. Kimuundo, ameweza kubainisha miundo changamani ya ushairi wa
Kiswahili na kupata mitindo anuai katika ushairi huu. Ameonesha ustadi wake katika
usanaji wa miundo na mitindo ya ushairi wa Kiswahili, ya zamani, ya sasa na mipya
hivyo kuupa hadhi ushairi huu.